Tuesday, December 18, 2012

UMUHIMU WA UDONGO MZURI



8 Nyingine zilianguka katika udongo mzuri, zikakua na kuzaa: moja punje thelathini, moja sitini na nyingine mia."  (Luka 4:8)


Tunahitaji kuzaa matunda yanayokaa. Katika hali ya kawaida bila udongo mzuri mazao hayatastawi kabisa. Pasipo udongo mzuri kukua ni ndoto za abunuasi. Pasipo udongo mzuri tusitegemee nguvu za Mungu. Pasipo udongo mzuri tusitegemee kujitoa kikamilifu kwa Yesu. Pasipo udongo mzuri hakuna kujaa na kufurika. Pasipo udongo mzuri tusitegemee uamsho kwa mtu au kwa kundi. Udongo upo wa aina nyingi. Hata wakulima wanapotaka kupanda mazao yao hawaendi popote tu wakapanda mbegu. Mkulima mzuri atachagua mahali panapofaa kwa mbegu zake kuota na kukua.


Je mimi na wewe tupo katika udongo gani? Je ni mfinyanzi? Je, ni mchanga, Je, ni udongo mzuri?


Maadamu mbegu ni mfano wa mtu, hakuna bahati mbaya katika kupandwa kwenye udongo usiofaa. Mtu mwenyewe anajipeleka kwenye udongo mzuri au ule usiofaa. Uchaguzi wa wapi ukapandwe kama mkristo ni wako wewe mwenyewe.


Ukitaka kukua na kuongezeka au kuzaa unajikita kwenye udongo mzuri. Ukitaka kuwa mkristo wa kawaida bila kuwa na matunda unajikita kwenye mwamba, kwenye miiba au popote pasipokuwezesha kukua na kuongezeka. Hii ni mada endelevu.


Barikiwa

KUOMBA KWA MUDA MREFU

Ombeni bila kukoma (1 Thes 5:17)

Mtu anapoanza kuokoka tunaweza kumfundisha kuomba au jambo fulani la kiroho kwa kutumia vikanuni na vijisheria fulani. hii ni kwa sababu yeye bado ni mchanga na anahitaji maziwa. Bado anahitaji kuelekezwa taratibu. 

Lakini ukiisha kuwa mzoefu wa maneno ya imani, au umeshakua kiroho haitakiwi ufundishwe kama wanaoanza safarileo. Mbinu ambayo mimi ninaishauri ni kutumia sifa, neno na kuabudu. Ukiwa kwako unaweza ukakesha bila taabu. Andaa tenzi, biblia kalamu daftari. Usiweke sana kanuni kuhusu nini kianze na nini kifuate.

Unafungua kwa maombi mkesha wako. Unaanza kuimba pambio mbalimbali za kusifu. Unafuatisha kuimba nyimbo za kuabudu. Ukiona roho yako imeloana uwepo anza kuomba kwa kufuata jinsi Roho Mtakatifu atakavyokuongoza. Kama ni kunena kwa lugha fuatisha tu. Ukiona umefanya chochote sana mpaka unakuwa kama umechoka acha na uanze kingine. Mfano acha kuomba, ingia kusifu. Hivyohivyo na itafika mahali ambapo hakuna anayeweza kukuzuia. Hapo unaweza kuomba hadi asubuhi. 

Wewe una maoni gani?

BARIKIWA


Sunday, December 16, 2012

FIMBO YA NGUVU ZAKO


Bwana atainyosha toka sayuni
Fimbo ya nguvu zako
Uwe na enzi kati ya adui zako. (zaburi 110:2)

 

Tunapoendelea kuishi katika maisha ya wokovu au utauwa, tunakutana na vikwazo, milima, visiki, mawe, magonjwa, njaa, kuishiwa, madeni, kuchukiwa, kuonewa, upinzani, kukosa uhuru na mengine mengi. Tunakutana na hayo kwa sababu hayo ni sahemu ya dunia tunayoishi. Hatupandishwi daraja bila kushinda katika hayo. Mwimba zaburi anaposema adui,  analenga vitu vyote nilivyotaja hapo juu. Mengine yameendelea kuwa changamoto kwetu hata wakati ambao tumeyakemea au kuomba yaondoke kabisa.

Pamoja na changamoto za namna moja au nyingine, neno la Mungu linatukumbusha kwamba tunayo fimbo. Hii ni alama ya mamlaka. Fimbo yako ni mamlaka yako. Ahadi imetolewa. Kama ukishaielewa ni ahadi ya jinsi gani na uidai vipi kwa Bwana basi utachangamka. Wewe dai ahadi ya fimbo yenye nguvu.

Fimbo hii itanyoshwa kutoka sayuni, na siyo kutoka Mabwepande au Makambako. Fimbo hii haitanyoshwa kama kubofya rimoti ya TV. Fimbo hii inatafutwa. Fimbo hii inahangaikiwa. Tunajua sana kwamba hata Yesu mwenyewe alisema kwamba ufalme wa Mungu utatekwa na wenye nguvu. Fimbo inanyoshwa kutoka Sayuni. Sayuni ni kwenye maombi. Sayuni ni kwenye ibada. Sayuni ni kwenye sifa. Sayuni ni kwenye maombi ya kujitoa. Sayuni ni kwenye kusoma neno.Sayuni ni katika kutafakari neno na kupata mafunuo.

Vitu nilivyovitaja hapo juu vinashindika tu mbele za Mungu kupitia Mfalme Yesu. Ni hiyo fimbo yenye nguvu inayoleta jibu kwako.

Tafakari

Thursday, December 13, 2012

UMWONE MUNGU BILA UTAKATIFU?


14 Jitahidini kuishi kwa amani na watu wote. Ishini maisha ya utakatifu, kwa sababu hakuna mtu atakayemwona Bwana bila ya maisha kama hayo( Waebrania 12:14)

Sisemi kwamba hujui kutubu ee ndugu katika bwana. Sisemi kuimba ni tatizo rafiki. Ila ninachosema ni kwamba, utakatifu wa kumuona Mungu unazingatia amani ya mtu na watu wote. Siku hizi ni vigumu kuhubiri injili ya utakatifu wote makanisani. Watu wako tayari kukuundia vikao vya kufukuzwa kanisani ikiwa tu utahubiri utakatifu kwa viwango vya juu. Watu waliookoka siku hizi tumepoteza sifa na maana ya kuokoka. lokole ndo wanaolalamika sana, hawamtegemei Mungu kama zamani. Hawavai vizuri na kwa heshima tena. Nywele zao huzitengeneza kama watu wa mataifa wanavyotengeneza. Yaani ni kukosa kiasi, ni kulata fujo tu humo makanisani.

Wewe unatengeneza nywele, una amani na Mungu wako sawa sikatai. Lakini hizo nywele ni kwazo kwa wanaokutazama au majirani zako.Pia ni kwazo kwa afya ya ngozi yako. Je amani yako na watu ikoje? unavaa pedo pusher, umejaa Roho Mtakatifu, sina tatizo. Hiyo amani ya pedo pusher kwa watu wote inapatikanaje?

Usifanye kitu kinacho poteza amani na watu wote. Kumbuka siyo mtu mmoja tu, ni watu wote. Suala siyo utakatifu tu, ila ni utakatifu ambatano. (Waebrania 12:14)

barikiwa

UPANDE WA BWANA

31 Kutokana na hayo, tuseme nini zaidi? Ikiwa Mungu yuko upande wetu, nani awezaye kutupinga?


Katika mchezo wa mpira wa miguu, kukiwa na upande wa Mungu na ule wa Ibilisi, ni vema kuchagua upande wa Mungu.

Kwenye upande wa Mungu kuna amani, uzima wokovu, neema, na baraka tele.

Ukiokoka unakuja upande wa Bwana.

Ukiwa huko kwa Bwana hakuna jambo lolote la kukutisha. Bwana akiwa upande wetu ni mchawi gani aliye juu yetu? ni umasikini gani ulio juu yetu? ni huzuni gani iliyo juu yetu? ni pepo gani ata kuwa juu yetu? ni freemason gani aliye juu yetu?

Ongeza mambo mbalimbali na utaona kwamba alipo Yehova hakuna kushindwa, hakuna udhaifu nk.

Barikiwa

UTAKATIFU WA KILA SIKU


 

kwa unyofu na uadilifu mbele yake, siku zote za maisha yetu. (Luka1:75)




Mara nyingi sana huwezi kukuta mtu aliyeokoka anfurahia dhambi. Hata hivyo ukweli unabaki palepele kwamba watu wengi tuna utakatifu wa mdomo na si ule wa matendo.

Kusema ukweli limekuwa jaribu kubwa nyakati za leo. Watu ni wakali na hawapendi kuguswa kwenye maeneo ya udhaifu wao.

Utakatifu katika andiko hilo hapo juu ni ule wa siku zote. Utakatifu wa masaa ni kinyume cha biblia. Utakatifu wa wiki siyo neno la Mungu. Utakatifu wa kuimba pambio tu, sicho tulichoitiwa.




Hapatakiwi kuwa na tofauti ya mahali katika suala la utakatifu. Kazini na nyumbani mtu uwe yule yule unayemcha Mungu.

OMBI:

Ee Mungu naomba unijalie kuwa na toba ya kweli kuhusu njia zangu. Naomba unielekeze katika kukuhofu wewe, na kuwa mtakatifu siku zote